Monsuni - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Monsuni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mawingu yanayoletwa na upepo wa monsuni karibu na mji wa Nagercoil, Uhindi.

Monsuni ni upepo wa majira unaoendelea kwa muda wa miezi kadhaa kuelekea upande mmoja na kubadilika baada ya kipindi hiki kuelekea kinyume.

Neno hili lilitumiwa mara ya kwanza katika eneo la Bahari Hindi [1] ambako inajirudiarudia kwa nguvu hasa.

Mabaharia Waswahili huwa na maneno tofauti, kutegemeana na mwelekeo wa upepo huo kimajira: musimi au kaskazi, na kusi au demani[2].

Monsuni inapeleka hewa yenye unyevu mwingi kutoka baharini hivyo kuwa na mvua nzito.

Sasa neno latumiwa pia kwa pepo zinazofuata utaratibu wa kufanana katika sehemu nyingine za dunia kama vile Asia ya Kusini-Mashariki au Amerika Kusini.

Monsuni hufuata mfumo wa msingi wa fizikia: nchi kavu hushika joto kutoka kwa jua haraka zaidi kuliko maji. Tofauti ya halijoto kati ya nchi kavu na bahari kwenye pwani unaweza kufikia kiwango cha sentigredi 20°C. Kwa mfano halijoto kwenye nchi kavu huko Uhindi inaweza kufikia mnamo 45°C ilhali maji ya karibu katika Ghuba ya Bengali na Bahari Arabu ina halijoto ya sentigredi 23-25 pekee. Joto la nchi kavu linapashia moto hewa juu yake na hewa joto inapanda juu. Nafasi ya hewa inayopanda juu inachukuliwa na hewa baridi zaidi kutoka juu ya uso wa bahari. Hewa hii inabeba unyevu ndani yake inayoanza kutonesha kama mvua unaojulikana kama monsuni.

Hewa joto juu ya nchi kavu inaendelea kupanda juu na kusababisha eneo la kanieneo ya hewa duni na hii inasababisha upepo wa kuendelea kutoka baharini kuelekea bara. [3]

Usimbishaji unaimarishwa na milima inayolazimisha hewa yenye unyevu kutoka uso wa bahari kupanda juu.[4]

Milima ya Ghat kwenye pwani ya magharibi ya Uhindi wakati wa Mei 2010 (majira ya monsuni ya kaskazini).
Milima ya Ghat kwenye pwani ya magharibi ya Uhindi wakati wa Agosti 2010 (majira ya monsuni ya kusini).

Wakati wa baridi nchi kavu hupoa haraka kuliko bahari inayoweza kutunza joto vizuri zaidi kwa muda mrefu. Hivyo eneo la kanieneo la hewa juu linatokea barani Uhindi wakati wa baridi na sasa upepo unageuka kupuliza kutoka bara Hindi kwenda baharini na upepo huu ni kavu.

Monsuni, mazingira na binadamu

[hariri | hariri chanzo]

Upepo wa monsuni unajenga tabianchi ya maeneo yanayoathiriwa nao inayoitwa pia "tabianchi ya monsuni".

Monsuni inaleta mvua nyingi ambayo mahali pengi ni msingi wa misitu. Mabadiliko ya monsuni yanaweza kuleta ama ukame mbaya au mvua kali zinazosababisha matatizo katika jamii.

Kwa hiyo monsuni ni muhimu kwa kilimo na maisha ya watu katika maeneo yanayoathiriwa nayo. Hasa katika nchi zinazozunguka Bahari Hindi majira ya monsuni yalikuwa msingi wa biashara kwa njia za bahari na kubadilishana kwa tamaduni kati ya nchi mbalimbali.

Tangu milenia watu walioishi kando ya Bahari Hindi walitumia upepo wa monsuni kwa safari zao. Monsuni ya kusini -iliyoitwa "kusi" au "upepo wa kusi" na Waswahili- iliwawezesha watu wa pwani kufanya safari ndefu sana za kuvuka bahari kati ya Uhindi, Bara Arabu na Afrika ya Mashariki kwenda upande mmoja hata kwa jahazi nyepesi sana, na badiliko la mwendo wa monsuni liliwawezesha kurudi tena majira yaliyofuata.

  1. Neno la Kiingereza monsoon linatokana na lile la Kireno monção, lilitokana na Kiarabu mawsim (موسم "majira") na/au Kihindi "mausam", "labda kwa kupitia pia Kiholanzi cha awali monsun". OED online
  2. Linganisha A.C. Madan, Eenglish-Swahili Dictionary, London 1902; TUKI-ESD imepokea "monsuni"
  3. Watts, Louisa 2009. What causes the west African monsoon? National Centre for Environmental Science. Retrieved on 2009-04-04.
  4. Pidwirny, Michael 2008. CHAPTER 8: Introduction to the Hydrosphere (e). Cloud Formation Processes. Physical Geography. Retrieved on 2009-01-01.